Img 20260927 Wa0007

Taifa Gas Yaendelea Kufanikisha Mkakati Wa Kitaifa Wa Matumizi Ya Nishati Safi

MUHTASARI


Yatoa motisha ya pikipiki kupitia kampeni ya Balozi wa Nishati


Katika jitihada za kufanikisha mkakati wa serikali  wa kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, Kampuni ya Taifa Gas imeendelea kutoa elimu katika jamii nchini ambapo mwishoni mwa wiki imetoa zawadi ya pikipiki kwa Bi. Pilly Zubery mkazi wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala kupitia kampeni yake ya Balozi wa Nishati iliyoanzishwa mwaka jana.

Kampeni ya Balozi wa nishati safi imelenga kuwawezesha na kuwahamasisha wananchi wa Msalala kutumia nishati safi ya gesi kwa ajili ya kupikia sambamba na kuwafanya mabalozi wa nishati hiyo katika maeneo yao na ilizinduliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo wananchi walipatiwa mafunzo ya nishati safi ya kupikia na mawakala 20 ambao ni mabalozi wa nishati kupatiwa mitungi 320 ya gesi kutoka kampuni ya Taifa Gas kwa ajili ya kusaidia katika uhamasishaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki hiyo Meneja Masoko wa kampuni ya Taifa Gas, Bwn. Oscar  Shelukindo amesema kuwa kampeni ya Balozi wa Nishati imepata mafanikio makubwa ambapo wananchi wengi wa Msalala hivi sasa wameachana na matumizi ya mkaa na kuni zisizo salama kwa mazingira na kiafya na kuanza kutumia nishati safi ya gesi.

Img 20260927 Wa0009
 Bwn Oscar Shelukindo

Alitoa pongezi kwa mshindi Bi.  Pilly Zubery kwa kuwa mhamasishaji mzuri ambaye amekuwa wakala na balozi  aliyeweza kufikisha elimu kwa kaya  zaidi ya 50 na kuzibadilisha kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo salama na  sasa zinatumia nishati safi na salama ya kupikia.

Shelukindo pia alitoa pongezi wa mabalozi wengine ambao wanaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na alishukuru mgodi wa Barrick Bulyanhulu ambao u,mekuwa mdau mkubwa katika kampeni na kutoa wito kwa wananchi wote wa Msalala kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo  ina gharama nafuu,inalinda mazingira na afya kwa watumiaji.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa Taifa Gas kanda ya ziwa Bi Hawa Omary alisema mwitikio wa matumizi ya nishati Halmashauri ya Msalala unazidi kuwa mkubwa ambapo kwa sasa wananchi wengi wameanza kutumia  gesi tofauti na hali iliyokuwa hapo awali kabla ya kuanzishwa kwa kampeni hii.

“Matokeo haya yanatia moyo na yanaonyesha dhamira ya Serikali kuhakikisha wananchi wanatumia nishati iliyo salama na yenye manufaa kwa afya na mazingira”alisema.

Mwakilishi wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu katika hafla hiyo,Mary Lupamba ambayi ni Afisa Mahusiano ya jamii alisema Barrick itaendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kulinda mazingira na kushirikiana  na wadau wengine wa kulinda mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Img 20260927 Wa0008
 Bi Pilly Zuberu akipokea kadi ya Pikipiki kutoka kwa Meneja Masoko wa Taifa Gas , Oscar Shelukindo (kulia) na kushoto ni Afisa Mahusiano wa Jamii wa Barrick Bulyanhulu baada ya Bi Pilly Zubery ambaye ni Balozi wa matumizi ya nishati kuweza kufikia kaya zaidi ya 50 kwenye kampeni hiyo

Naye mshindi wa zawadi ya pikipiki  Pili Zubery alishukuru waandaaji wa kampeni hii ya Balozi wa Nishati ambayo mbali na kuhamasisha nishati safi imeweza kuwa mkombozi wa wanawake ambao walikuwa wanatumia muda mwingi na nguvu kutafuta nishati ya kupikia pia imeweza kuwainua kiuchumi katika biashara zao ndogondogo.

“Wakati naanza biashara sikuwa na mtaji mkubwa lakini kutokana na mafunzo tuliyopatiwa na Taifa Gas kuhusu matumzi ya nishati safi niliweza kutembelea kaya nyingi na kutoa elimu niliyoipata na kuwezesha kaya zaidi ya 50 ku badilika kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo salama.

“Nashukuru kwa kupewa zawadi ya pikipiki ambaye imekatiwa na bima ambayo nitaitumia katika kurahisisha biashara zangu katika usambazaji na kuwafikia wateja wengi zaidi,” alieleza.

Serikali ilizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia mnamo Mei 8, 2024, ikilenga kufikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034, au hata asilimia 75 ifikapo 2030.

Kampuni ya Taifa inazidi kuwa kinara wa kufanikisha mkakati huu ambapo inaendelea kupeleke elimu na huduma katika mikoa yote nchini.

Kampeni ya matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia ilianzishwa kitaifa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika juhudi za kuhakikisha watanzania hasa wanawake wanaondokana na matumizi ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia.

Img 20260926 Wa0004 Previous post NHIF, Hospitali Ya Aga Khan Zaingia Makubaliano Matibabu Ya Wagonjwa Wa Saratani 
Img 20260928 Wa0014 Next post Serikali Yafanya Kikao Kazi Cha Kukabiliana Na Mvua Za EL Nino:  Ziara Kufanyika Nchi Nzima Kukagua Utayari Wa Kukabiliana Na Athari Za Mvua Zinazotarajiwa