MUHTASARI
Ni kutokana na ufanikishaji wa ujenzi wa shule mpya ya msingi kijijini Kerende
Uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini unaendelea kunufaisha jamii zinazozunguka maeneo ya mgodi wake wa North Mara wilayani Tarime ambapo kupitia fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ambapo karibuni umefanikisha mradi wa ujenzi wa shule ya msingi mpya ya kisasa katika kijiji cha Kerende kilichopo kata ya Kemambo wilayani Tarime, ambayo itawezesha mamia wanafunzi kuanza kupata elimu ya msingi bila kutembea umbali mrefu.
Kijiji cha Kerende kina vitongoji 10 ambapo wanafunzi kutoka vitongoji vitatu vya Mgosi, Isakahembe na Nyanyoka watakuwa wanufaika wa shule hiyo mpya ambayo itakuwa ya nne katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 8,000, na imepewa jina la Mlima Mgosi ambao ni moja ya kivutio kilichopo katika kijijini hapo.
Mradi wa ujenzi wa shule hiyo ulianza Juni 2025 na mkandarasi wake aliukabidhi kwa Serikali ya Kijiji hicho Januari 2026 na taarifa zilizopo zinasema maandalizi ya kufungua shule hiyo yapo katika hatua za mwisho na wakati wowote itafungua milango kwa mamia ya wanafunzi ambao watahamishwa kutoka shule nyingine zilizopo katika kijiji hicho.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerende, Bwn. Marwa Gabogwe ameeleza kuwa mradi huu wa kuboresha elimu kijijini hapo umeenda vizuri na utafanikisha kuwezesha wanafunzi wengi kujiunga na elimu ya shule ya msingi na kwa kiasi kikubwa umewaondolea adha wanafunzi wa kijiji hicho kutembea umbali wa mwendo mrefu kutafuta elimu katika shule zilizopo vijiji vya mbali.
Shule nyingine za msingi za serikali zilizopo katika kijiji hicho ni Kerende, Ngeng’e na Ntimaro.
Shilingi zaidi ya milioni 300 zimetumika katika kutekeleza mradi huo ambao umehusisha ununuzi wa uwanja wa eneo la shule (ekari 10), ujenzi wa vyumba sita vya madarasa, ofisi ya walimu, vyoo vya walimu, wanafunzi na uwanja wa mpira.
Utekelezaji wa mradi huo pia umejumuisha utengenezaji wa madawati ya wanafunzi 125 ambayo yapo tayari yakisubiri wanafunzi watakaofungua pazia katika shule hiyo.
Wakazi wa kijiji cha Kerende wanatoa shukrani kwa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals kwa kutoa fedha ambazo zimefanikisha ujenzi wa shule hiyo kupitia mpango wake wa CSR.
“Mradi huu ulikuwa hitaji kubwa kwa sababu kijiji chetu kina vitongoji 10 na wanafunzi ni wengi. Hivyo, itakuwa na msaada mkubwa kwa watoto wetu,” anasema mkazi wa kijiji hicho, Bwn. Mussa Magaigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kerende.
Naye Diwani wa Kata ya Kemambo, Bwn. Rashid Bogomba, anasema ujenzi wa Shule ya Msingi Mgosi katika kijiji cha Kerende ni sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mipya inayofadhiliwa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia sera na kanuni ya CSR.
“Kazi inaendelea vizuri, fedha za CSR zimejenga shule mpya ya msingi Mgosi na majengo yote yamekamilika, haya ni maendeleo makubwa,” anasema Bwn. Bogomba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa Barrick North Mara.

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Mgodi wa North Mara umetumia shilingi bilioni 26.86 kufanikisha utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime tangu mwaka 2019 Barrick ilipoanza kuendesha shughuli zake nchini kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Miradi mikubwa ya CSR iliyofanikishwa na Barrick North Mara iko katika sekta ya elimu,maji safi kwa wananchi,afya,ujenzi wa miundombinu ya barabara na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
