MUHTASARI
Shilingi bilioni 117.52 zitakusanywa kupitia tozo za magari ya kigeni yaingiayo nchini (transit charges).
BODI ya Mfuko wa Barabara (RFB) inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 999.40 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake muhimu, ikiwemo kugharamia miradi ya matengenezo ya barabara katika mikoa mbalimbali nchini katika mwaka wa fedha 2026/27.
Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kupatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyohusiana na shughuli za Bodi, ikiwemu tozo za matumizi ya miundombinu ya barabara.
Akizungumza wakati wa mahojiano maalumu na Mwafrika jijini Dodoma, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, alisema Shilingi bilioni 816.34 zinatarajiwa kupatikana kutokana na makusanyo ya tozo ya mafuta, Shilingi bilioni 117.52 zitakusanywa kupitia tozo za magari ya kigeni yaingiayo nchini (transit charges), huku kiasi cha Shilingi bilioni 65.52 zikitarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vingine, ikiwemo tozo za mizigo yenye uzito au vipimo visivyo vya kawaida.

Alisema bajeti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 ni sawa na asilimia 28 ya mahitaji yote ya fedha kwa ajili ya kuhudumia barabara za kitaifa na wilaya yaliyowasilishwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA).
“Chini ya bajeti hii, barabara ambazo kwa sasa ziko katika hali nzuri zimepewa kipaumbele, ambapo asilimia 100 ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya matengenezo zimetengwa ili kuhakikisha barabara hizo zinaendelea kuwa katika hali nzuri na haziharibiki,” alisema.
Aidha, alisema kipaumbele kitatolewa kwa barabara zenye kiwango kikubwa cha matumizi na zinazohudumia vituo muhimu vya kiuchumi, kijamii na kiutawala.
“Barabara hizo zinajumuisha korido kuu za kiuchumi za kitaifa kama TANZAM na Central Corridor, kwa kuwa zinahudumia bandari za Tanzania, pamoja na barabara zinazohudumia miji mikubwa, maeneo ya kilimo, vituo vya utalii na madini, maeneo ya viwanda, hospitali na vituo vya elimu,” alisema.
Alisema katika mwaka wa fedha uliopita wa 2025/26, Bodi ya Mfuko wa Barabara ililenga kukusanya Shilingi bilioni 986.28 kutokana na tozo na ushuru wa matumizi ya barabara.
Hata hivyo, alisema Bodi ilifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 1,221.23, sawa na asilimia 140 ya makadirio ya makusanyo yaliyokadiriwa.
Kuhusu tozo za magari yanayopita nchini, alisema magari yenye ekseli hadi tatu hutozwa Dola za Marekani sita kwa kila kilomita 100, wakati magari yenye ekseli zaidi ya tatu hutozwa Dola 10 kwa kila kilomita 100.
“Kwa kupitia tozo hizi, watumiaji wa barabara wanachangia gharama za matengenezo ya barabara, hivyo kufidia uchakavu unaosababishwa na matumizi ya magari yao kwenye barabara,” alisema.
Hata hivyo, alisema Bodi inakabiliwa na changamoto kadhaa katika ukusanyaji wa tozo na ushuru unaohusiana na miundombinu ya barabara.
Alitaja uwepo wa mifumo mingi ya kisheria pamoja na tafsiri tofauti za sheria zinazotolewa na mamlaka za serikali za mitaa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri ukusanyaji wa mapato.
“Mifumo mingi ya kielektroniki ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, pamoja na uwezo mdogo wa kifedha na kiufundi wa kuwekeza katika vituo vya kuzalisha mapato, kama maeneo maalumu ya maegesho ya malori, ni miongoni mwa changamoto nyingine zinazoathiri ukusanyaji wa tozo na ushuru unaohusiana na miundombinu ya barabara,” alibainisha.

Pia alitaja upungufu wa rasilimali watu kuwa changamoto nyingine inayoathiri usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato katika mikoa yote nchini.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Mfuko wa Barabara imeziagiza TANROADS na TARURA kuandaa na kuwasilisha mikakati ya kuzuia au kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara unaoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kuanza kunyesha mwezi huu.
Bodi pia imeziagiza taasisi za barabara nchini kuhakikisha miundombinu ya kupitisha maji, ikiwemo makaravati, inakuwa wazi ili kuruhusu maji kutiririka kwa uhuru.
“Pia tumewashauri kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kugharamia kazi muhimu za dharura zitakazohitajika kurejesha ubora wa miundombinu ya barabara endapo kutatokea uharibifu wakati wa mvua,” alisema Mhandisi Kalimbaga.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa sera ya Bodi ya Mfuko wa Barabara, kuhusu usimamizi wa kazi za dharura za matengenezo ya barabara, TANROADS na TARURA zinatakiwa kutenga asilimia tano ya bajeti zao kwa ajili ya kugharamia kazi hizo.
“Katika mwaka wa fedha 2026/27, jumla ya Shilingi bilioni 38 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia kazi za dharura katika barabara za kitaifa na wilaya,” alisema.
Alieleza kuwa miongoni mwa malengo ambayo Bodi inalenga kuyafikia ili kuboresha ufanisi wa utendaji wake ni kuongeza matumizi ya teknolojia katika shughuli zake za kila siku na kuimarisha uwezo wa watumishi kupitia programu za mafunzo.
