MUHTASARI
Mashindano yanayofanyika katika mazingira ya misitu yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa vitendo kuhusu thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, amesema michezo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu na mazingira, akisema watu huwa na uelewa zaidi wanapoweza kuona na kunufaika na rasilimali hizo.
Makonda, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, alisema hayo, Oktoba 3, 2026, wakati wa ziara yake katika eneo la mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yanayofanyika Shamba la Miti Morogoro, ambapo pia alitembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na kupata maelezo kuhusu shughuli za uhifadhi zinazotekelezwa na Wakala huo.

Alisema mashindano yanayofanyika katika mazingira ya misitu yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza kwa vitendo kuhusu thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda.
“Ni jambo la kujifunza kwa kuona. Ukijifunza kwa vitendo unapata fursa kubwa zaidi ya kuelewa,” alisema.
Makonda alisisitiza kuwa misitu ina mchango muhimu katika maisha ya wananchi, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa mvua na mazingira bora ya kuishi, hivyo jamii inapaswa kuendelea kunufaika nayo huku ikilinda rasilimali hizo.
Aliwahimiza Watanzania kuwa walinzi wa misitu kwa kutambua thamani yake na kushiriki kikamilifu katika kuilinda dhidi ya uharibifu, akisisitiza kuwa manufaa yanayotokana na misitu yanaweza kuendelea kupatikana iwapo rasilimali hizo zitatunzwa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Salome Kivuyo, Afisa Utalii wa TFS, amesema TFS inaendelea kuwashirikisha wadau na wafadhili katika kuendeleza michezo ndani ya maeneo ya misitu kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi, ikiwemo mbio za baiskeli, pikipiki na marathon, kwa lengo la kuunganisha michezo na uhifadhi wa mazingira.
“Tunawakaribisha wadau mbalimbali waje tushirikiane katika kuleta michezo ndani ya misitu yetu, ili kuwapa Watanzania fursa ya kufurahia michezo hiyo, huku wakijifunza, kutambua na kuthamini thamani ya misitu na umuhimu wa kuilinda,” alisema Kivuyo.
Mashindano ya Serengeti Rally of Tanzania 2026 yanayoendelea katika eneo la Shamba la Miti Morogoro, linalosimamiwa na TFS, yamekuwa fursa ya kuunganisha michezo, uhifadhi, utalii na elimu ya mazingira, huku TFS ikitumia uwepo wake katika mashindano hayo kuwafikia wananchi na wadau kwa ujumbe wa uhifadhi na kuonesha namna misitu inavyoweza kutumika kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na kitalii kwa kuzingatia taratibu za uhifadhi.
Akizungumzia mashindano hayo, alisema amefurahishwa na maandalizi yake na namna yanavyofanyika katika mazingira ya Shamba la Miti Morogoro, akisema kuunganisha michezo na uhifadhi kunaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na wakati huo huo kukuza michezo na utalii.
