Img 20261108 Wa0010

ROSTAM AZIZI: Kampuni Za Kitanzania Zijengewe Mazingira Ya Kukua Kupitia Miradi Mikubwa Ya Uwekezaji Nchini

MUHTASARI


‘Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu lakini sehemu kubwa ya mikataba mikubwa inaendelea kutekelezwa na kampuni za kigeni, huku wakandarasi wetu wengi wakibaki na kazi ndogo ndogo hali inayosababisha waendelee kudumaa,”Bwn ROSTAM AZIZ


Mwenyekiti wa Taifa Group, Bwn Rostam Azizi ametoa rai kwa Serikali na wadau mbalimbali kuweka maslahi mbele katika suala la uwezeshaji watanzania ili kuwawezesha kumiliki uchumi wa nchi kama ambavyo wizara ya madini imeanza kutekeleza  na kusimamia sheria za kuwawezesha watanzania kushiriki na kunufaika na rasilimali za madini kupitia kanuni ya maudhui ya ndani ya ushirikishwaji watanzania katika mnyororo wa  thamani wa madini (Local content).

Akiongea katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Sekta za Ujenzi na Madini  (ACAMEA 2026)  iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo alikuwa mgeni rasmi, Bwn Rostam Azizi alisema Tanzania ina fursa nyingi za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na madini na ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu, na pia nchi ina idadi kubwa ya vijana wenye uwezo na ari ya kufanya kazi, ambapo ametaadharisha kuwa wasipojengewa mazingira mazuri fursa hizi hazitanufaisha vijana wa kitanzania na hatutakuwa na makampuni imara nchini.

Alisema jukumu la uwezeshaji  watanzania kiuchumi sio la serikali pekee bali linahusu sekta binafsi, taasisi za fedha, wakandarasi na wataalamu wetu.

Img 20261108 Wa0009
Mfanyabiashara maarufu na Mwenyekiti wa Taifa Group nchini , Rostam Azizi akizungumza kwenye hafla ya tuzo za umahiri katika sekta za Madini na Ujenzi (ACAMEA 2026) ambapo alisisitiza umuhimu wa watanzania kujengewa uwezo kwa kupatiwa miradi mikubwa ya ujenzi ili waweze kupata uzoefu.

“Serikali ina nafasi ya kuwa na sera wezeshi na kutengeneza mazingira yanayotoa fursa sawa kwa wote, Taasisi za fedha zina nafasi ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji. Na kampuni zetu zina wajibu wa kujenga uwezo, kuzingatia ubora na kutekeleza kazi kwa uadilifu” Alisema.

Azizi alisema tusiridhike kujenga barabara bila kujenga wakandarasi wetu, au kujenga reli bila kujenga kampuni zenye uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa au kuchimba madini bila kujenga uwezo wa Watanzania kumiliki sehemu kubwa zaidi ya uchumi unaotokana na rasilimali hiyo.

 “Tunaposherehekea washindi wa ACAMEA leo, tusheherekee pia uwezo wao wa kufanya makubwa zaidi huko mbeleni. Tujiulize sisi, kama Serikali, wawekezaji na viongozi wa sekta hizi, tunafanya nini kuhakikisha uwezo huo hauishii hapa. Miundombinu tunayojenga leo itakuwa urithi wa vizazi vijavyo. Lakini urithi mkubwa zaidi utakuwa uwezo wa Watanzania kuujenga, kuumiliki na kuuendeleza uchumi wao wenyewe” Alisisitiza.

Alisema maswali ya kujiuliza kupitia miradi mikubwa inayojengwa nchini ya barabara, reli, madaraja, mabwawa na miundombinu mingine mikubwa tunajenga kampuni kubwa za Kitanzania? Na fedha nyingi kutumika kujenga miradi hiyo ni kampuni ngapi za Kitanzania zimekua? Ni wakandarasi wangapi wamejenga uwezo mpya? Na ni utaalamu gani utabaki nchini kwa ajili ya miradi ya baadae? 

Na kusisitiza kuwa maendeleo hayatokani tu na kukamilisha miradi bali ni pamoja na kujenga uwezo wa Watanzania kutekeleza miradi hiyo wenyewe.

Azizi alihoji kuwa kama Wizara ya Madini imethubutu kuchukua hatua za makusudi za kuwalinda na kuwawezesha Watanzania, kwa nini tusifanye hivyo hivyo katika sekta ya ujenzi na sekta nyingine za uchumi wetu? Na kusema kuwa madini sio suala la mapato na ajira tu, bali pia ni suala la kujenga kampuni imara za Kitanzania, viwanda, teknolojia, wataalamu na kukuza mitaji ili kuendelea kuzalisha thamani hata baada ya madini kuisha.

“ Thamani ya madini haipo tu kwenye kile tunachokichimba ardhini. Ipo pia kwenye uhandisi, mitambo, teknolojia, usimamizi na biashara zinazozunguka shughuli za uchimbaji. Hizi ni fursa ambazo Watanzania wanapaswa kuzitumia kujenga uwezo wa kampuni zao” Alisema.

Aidha, aliipongeza serikali kupitia wizara ya madini kwa hatua ambazo imezichukua ili kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hii kupitia sera, sheria na kanuni za ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa uchimbaji madini, yakiwemo marekebisho ya mwaka 2025, ambayo yanaendelea kuongeza fursa za kampuni za Kitanzania kushiriki katika shughuli za uchimbaji na huduma mbalimbali zinazohusiana na migodi.

Azizi alitoa rai ya kuondokana na dhana ya kuyaona makampuni ya kitanzania kuwa hayana uwezo wa kufanya kazi kubwa maana kampuni haikui kwa kutamani ikue tu bali inakua kwa kupata kazi, kujenga uzoefu, kukusanya mtaji na kuwekeza lakini ili kampuni ipate kazi, lazima kwanza kuwe na mtu anayeamini kwamba inaweza kuifanya kazi hiyo na  hapa ndipo kuna tatizo kwa kuwa Watanzania hatuaminiani.

Img 20261108 Wa0011
Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Taifa Group , Rostam Azizi akipokea tuzo ya heshima  kutoka kwa Mwenyekiti mwasisi wa Tamisa , Peter Kumalilwa kwa kutambua mchango wake kwenye sekta ya madini na ujenzi kama mtanzania mzawa.

“Si kila kampuni ya Kitanzania ina uwezo wa kutekeleza kila mradi mkubwa. Miradi mikubwa inahitaji utaalamu, mitaji, teknolojia na usimamizi wa hali ya juu. Hilo halina ubishi.Lakini hilo halimaanishi kwamba hakuna kampuni za Kitanzania zenye uwezo. Na pale ambapo uwezo haujatosha, tunapaswa kuwa na mkakati wa kuujenga, kama ni mitambo, inaweza kununuliwa au kukodishwa. Wataalamu wanaweza kuajiriwa. Teknolojia inaweza kupatikana. Ubia unaweza kuundwa.  Uzoefu unajengwa kwa kufanya kazi, hatuwezi kuendelea kusema kwamba wakandarasi wetu hawana uwezo, wakati hatuwapi fursa za kuujenga uwezo huo. Uzoefu haupatikani kwa kusubiri. Unapatikana kwa kufanya kazi,” Aliongeza.

Kuhusu kupata wakandarasi wa kutekeleza miradi mikubwa nchini, Rostam alishauri kuwa uwezo wa mkandarasi usipimwe kwa jina, uraia wake au lugha anayoizungumza bali upimwe kwa kwa wataalamu wake, uwezo wake wa kifedha, rekodi ya utekelezaji, usalama na ubora wa kazi zake na tusimdharau mkandarasi wa Kitanzania kwa sababu tu anazungumza Kiswahili na  kuondokana na dhana kuwa mkandarasi kutoka nje anao uwezo mkubwa zaidi kwa sababu tu anazungumza lugha ya kigeni na kampuni zote Na hapa, ninaomba nisieleweke vibaya.

Alisema hapingani na kampuni za kigeni kwa kuwa zina nafasi yake na utaalamu na teknolojia zinazoleta nchini zinahitajika bali anapingana na dhana kwamba kampuni ya kigeni ina uwezo kwa sababu ni ya kigeni, na kampuni ya Kitanzania haina uwezo kwa sababu ni ya Kitanzania.

Alisema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu lakini sehemu kubwa ya mikataba mikubwa inaendelea kutekelezwa na kampuni za kigeni, huku wakandarasi wetu wengi wakibaki na kazi ndogo ndogo hali inayosababisha waendelee kudumaa wakiwa pia wanakabiliwa na changamoto ya kucheleweshewa malipo baada ya kufanya kazi na kupelekea kampuni zenye uwezo kuwa kwenye hatari ya kufilisika.

Azizi alishauri kuwa ili kampuni zetu za kitanzania ziimarike kunahitajika sera na mfumo wa kisheria unaowapa wakandarasi wetu fursa za kweli, unaolinda ushindani wa haki na unaowajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa.

“Tusijenge uchumi wa dola trilioni moja ambao vijana wetu watakuwa watazamaji.Tujenge uchumi ambao vijana hawa watakuwa washiriki, viongozi na wamiliki. Kwa sababu mustakabali wa uchumi wetu hautategemea tu kiwango cha uwekezaji tutakachovutia, bali pia uwezo wa Watanzania kushiriki, kuongoza na kumiliki sehemu ya uchumi huo.” Alisisitiza.

Azizi aliwapongeza washindi wa tuzo za ACAMEA na kuitaka iendelee kuwa jukwaa linalounganisha kampuni zenye uwezo na fursa za miradi, taasisi za fedha, teknolojia na washirika wanaoweza kuzisaidia kukua.

“Ningependa kuona katika miaka ijayo kampuni tunazozitambua hapa leo zikiwa zimekua, zikiwa na mitaji mikubwa zaidi, zikiwa zimeajiri Watanzania wengi zaidi na zikiwa na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa zaidi.” Alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa masoko na Uhamasishaji Mitaji Chama cha Wadhamini Sekta ya Madini Tanzania (Tamisa), Dk Sebastian Ndege amesema hafla hiyo imehusisha wadau mbalimbali wakiwemo wa taasisi za madini, taasisi za fedha na wadau wengine.  Taifa group, NMB, Clouds media, TPSF, Blue coast nk.

Dk Ndege amesema hafla hiyo imehusisha sekta mbili, Sekta ya Madini na sekta ya ujenzi.

“Madini yanatoa rasilimali na ujenzi unatoa rasilimali hizo, tunapoelekea ubora huu, tunasherehekea yote hayo,” Amesema.

Img 20261108 Wa0013
Washiriki wa Tuzo za umahiri katika sekta ya Ujenzi na Madini wakiwa na tuzo zao.

 

Img 20261025 Wa0005 Previous post Afrika Yashauriwa Kuwekeza Kwenye Teknolojia Ya Nyuklia Kwa Maendeleo Endelevu