MUHTASARI
Dira ya 2050 inalenga kuongeza mchango wa Sekta ya Uvuvi katika Pato la Taifa kutoka wastani wa takribani asilimia 1.7 hadi zaidi ya asilimia 3 ifikapo mwaka 2050.
Na Herry Kilele – TAFIRI
Katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2050, Sekta ya Uvuvi imepewa nafasi ya kimkakati kama mojawapo ya nguzo muhimu za kukuza pato la Taifa, kuongeza ajira, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika muktadha huo, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeutambua utafiti, teknolojia na ubunifu kuwa nyenzo muhimu katika kuleta mageuzi kwenye Sekta ya Uvuvi na rasilimali za uvuvi. Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inatarajiwa kuwa miongoni mwa Taasisi zitakazochochea mageuzi hayo kupitia tafiti zinazolenga kuongeza tija, matumizi endelevu ya rasilimali na kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imejengwa katika nguzo kuu tatu ambazo ni uchumi imara, jumuishi na shindani, uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, pamoja na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
UCHUMI IMARA, JUMUISHI NA SHINDANI
Nguzo ya kwanza inalenga kujenga Taifa lenye uchumi imara na shindani, unaofungua fursa za kiuchumi, kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wananchi.
Tanzania imeendelea kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi, ambapo uchumi umekua kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa mwaka katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Dira ya 2050 inalenga kujenga uchumi mseto, shirikishi na wenye ushindani wa kimataifa, unaotumia ipasavyo rasilimali za ndani na kuendeshwa kwa sera madhubuti, mifumo bora ya udhibiti, biashara na ujasiriamali.

Katika kufikia azma hiyo, Sekta ya Uvuvi ina nafasi kubwa kutokana na uwezo wake wa uhakika wa chakula na afya, ajira, mapato na malighafi kwa viwanda.
UWEZO WA WATU NA MAENDELEO YA JAMII
Nguzo ya pili inalenga kujenga watu wenye uwezo, ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Dira ya 2050 inasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika malezi bora ya watoto, elimu na mafunzo, huduma za afya pamoja na mifumo imara ya hifadhi ya jamii.
Katika Sekta ya Uvuvi, kujenga uwezo wa wavuvi, wafugaji wa samaki, watafiti, wachakataji na wadau wengine ni jambo muhimu katika kuongeza tija na ushindani. Utafiti unaofanywa na TAFIRI unaweza kuwa daraja muhimu la kuunganisha maarifa ya kisayansi na mahitaji halisi ya wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki.
UHIFADHI WA MAZINGIRA NA USTAHIMILIVU WA MABADILIKO YA TABIANCHI.
Nguzo ya tatu inahusu uhifadhi wa mazingira na kuongeza uwezo wa Taifa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania imejaaliwa utajiri mkubwa wa maliasili na bioanuwai unaopatikana katika mifumo mbalimbali ya ikolojia, ikiwemo misitu, mito, maziwa na bahari. Rasilimali hizo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini zinahitaji usimamizi madhubuti ili ziendelee kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wa uvuvi, utafiti ni muhimu katika kufahamu hali ya rasilimali za uvuvi, mazalia ya samaki, mabadiliko ya mazingira na athari za tabianchi. Maarifa hayo yanaweza kusaidia Serikali na wadau kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali hizo.
TAFIRI NA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050
Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt. Ismael Kimirei, anasema Dira ya Maendeleo ya 2050 inasisitiza TAFIRI, pamoja na Taasisi nyingine za utafiti nchini zina nafasi ya kufanya utafiti, matumizi ya teknolojia na ubunifu wa kisayansi ili kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza tija na kutoa elimu kwa wadau.
Kwa mujibu wa Dkt. Kimirei, juhudi hizo zinalenga kujenga uchumi wa buluu na Sekta ya Uvuvi yenye uwezo mkubwa wa kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Katika sura inayohusu Kilimo, Uvuvi na Maliasili, Dira ya 2050 imeweka msisitizo katika kuchochea utafiti na ubunifu wa kisayansi kwa ajili ya kuboresha uzalishaji na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi.
KUONGEZA MCHANGO WA SEKTA YA UVUVI KATIKA UCHUMI.
Dira ya 2050 inalenga kuongeza mchango wa Sekta ya Uvuvi katika Pato la Taifa kutoka wastani wa takribani asilimia 1.7 hadi zaidi ya asilimia 3 ifikapo mwaka 2050.
Ili kufikia lengo hilo, tafiti za kisayansi zinahitajika katika kubaini maeneo yenye tija kwa uzalishaji wa rasilimali za uvuvi, kutathmini hali ya mazalia ya samaki, kuendeleza teknolojia bora za ufugaji wa samaki na kuboresha uchakataji pamoja na uongezaji thamani wa mazao ya uvuvi.
Hii ina maana kwamba matokeo ya tafiti yanapaswa kutafsiriwa kuwa teknolojia na maarifa yanayoweza kutumiwa moja kwa moja na wavuvi, wakuzaji viumbe maji, wawekezaji na wadau wengine.
Sekta ya Uvuvi imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa letu ambapo katika mwaka 2024, Sekta hii ilichangia asilimia 1.6 ya Pato la Taifa (GDP) na kukua kwa asilimia 2.3.
Aidha, katika kuimarisha Uchumi wa nchi, kuongeza fursa za ajira na kupunguza umaskini kwa mtu mmoja mmoja, Sekta ya Uvuvi imeendelea kunufaisha watanzania wapatao milioni 6 katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Uvuvi, wakiwemo wavuvi 205,559 na wakuzaji wa viumbemaji 53,992.
TAKWIMU SAHIHI KWA MAAMUZI SAHIHI
Mbali na kufanya tafiti, TAFIRI ina jukumu muhimu katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu sahihi na za wakati husika na kushauri usimamizi wa rasilimali za uvuvi.
Dkt. Kimirei anaeleza kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati ni msingi wa kufanya maamuzi bora na sahihi ya kisera, kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuongeza ushindani wa kiuchumi.
Takwimu kuhusu hali ya rasilimali za uvuvi, uzalishaji, ufugaji wa samaki na mwenendo wa sekta kwa ujumla zinaweza kusaidia Serikali kupanga mipango na sera zinazozingatia Ushahidi pamoja na mikakati ya usimamizi.
MASHIRIKIANO YA KIMATAIFA
Dira ya 2050 pia inasisitiza umuhimu wa mashirikiano mathubuti nay a kuleta tija kati ya Taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.
TAFIRI tayari inashirikiana na Taasisi mbalimbali, zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Taasisi ya Jiografia na Limnolojia ya Nanjing nchini China, Taasisi ya Korea ya Sayansi na Teknolojia ya Bahari (KIOST), pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Wildlife Conservation Society (WCS), Western Indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA), World Wide Fund for Nature (WWF), Shirika la Usimamizi wa rasilimali za Uvuvi Ziwa Victoria (LVFO), EAWAG, Chuo Kikuu cha Bern, Chuo Kikuu cha Kentucky, EAF-Nansen Programme, International Union for Conservation of Nature (IUCN), The Nature Conservancy (TNC), Bank ya Dunia (WB), Shirika la Chakula Duniani (FAO), WorldFish (an international research organization focused on aquatic food systems).
Mashirikiano haya yanatoa nafasi ya kubadilishana wataalamu, teknolojia na mbinu za kisasa za utafiti. Aidha, yanaweza kusaidia kuimarisha maabara na vituo vya utafiti, kuongeza upatikanaji wa vifaa na rasilimali fedha, pamoja na kujenga kizazi kipya cha watafiti wabobezi katika sayansi ya uvuvi na rasilimali za Uvuvi.
Muhimu zaidi, mashirikiano yanaweza kusaidia kuhakikisha matokeo ya tafiti hayabaki kwenye machapisho ya kitaalamu pekee, bali yanawafikia walengwa na kutumika kuboresha uzalishaji, usimamizi na masoko ya mazao ya uvuvi.
KUTOKA MAABARA HADI KWA MVUVI
Kwa mtazamo mpana, mafanikio ya Dira ya 2050 katika Sekta ya Uvuvi yatategemea uwezo wa Tanzania kubadilisha maarifa ya kisayansi kuwa suluhisho zinazoweza kutumika katika maisha halisi.

Teknolojia bora za ufugaji wa samaki, mbinu za kisasa za uvuvi, uhifadhi wa mazao, uchakataji na uongezaji thamani vinaweza kuongeza tija na mapato kwa wananchi, huku vikichochea uwekezaji na ajira.
Hivyo, jukumu la TAFIRI si kufanya utafiti pekee, bali pia kuhakikisha matokeo yake yanatoka kwenye maabara kwenda kwa wadau wa sekta ya Uvuvi wakiwemo wavuvi, wafugaji wa samaki, wachakataji, wawekezaji, wasimamizi na watunga sera.
HITIMISHO
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka msingi wa mageuzi makubwa katika Sekta ya Uvuvi kupitia utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia.
Katika safari hiyo, TAFIRI ina nafasi ya kimkakati kama chanzo cha taarifa, maarifa na takwimu sahihi, kitovu cha utafiti na ubunifu, pamoja na daraja linalounganisha sayansi na utekelezaji wa sera.
Iwapo tafiti zitawezeshwa ipasavyo na matokeo yake kutumika katika uzalishaji, usimamizi wa rasilimali na uongezaji thamani, Sekta ya Uvuvi inaweza kuwa miongoni mwa injini muhimu za kujenga uchumi imara unaolenga ushindani, ajira endelevu, usalama wa chakula na afya, na ustawi wa Watanzania ifikapo mwaka 2050.
