MUHTASARI
Baadhi ya wachimbaji huanza kutumia fedha nyingi katika uchimbaji bila kufanya utafiti wa kutosha wa eneo husika.
Kutumia utafiti wa kisayansi kabla ya kuanza uchimbaji wa madini kunaweza kusaidia wachimbaji na wawekezaji kupata taarifa sahihi kuhusu maeneo yanayolengwa kuanza uchimbaji na kupunguza matumizi ya fedha katika shughuli ambazo hazijathibitishwa kuwa na uwezekano wa kupata madini.
Akizungumza katika Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Mjiolojia na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Machimbo Explorer, Bwn David Mpanda Bembeja, amesema baadhi ya wachimbaji huanza kutumia fedha nyingi katika uchimbaji bila kufanya utafiti wa kutosha wa eneo.

Amesema utafiti wa madini unaweza kufanyika kwa kutumia geological, geochemical na geophysical surveys, kulingana na aina ya eneo na madini yanayolengwa, hatua inayosaidia kupata taarifa muhimu kabla ya kuanza uchimbaji.
Bembeja ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kukamilisha mchakato wa Bodi ya Wanajiolojia, ili wataalamu wa taaluma hiyo watambulike na kufanya kazi kwa kufuata miongozo inayotakiwa.
Amesema uwepo wa watu ambao si wataalamu sahihi wanaofanya kazi za kijiolojia na kuandaa ripoti zisizo sahihi unaweza kusababisha wawekezaji kupata hasara, hivyo kuwepo kwa bodi kutasaidia wataalamu kufanya kazi kwa uhalali na ripoti zao kutambulika kisheria.
Amesema Machimbo Explorer huanza kwa kuchambua leseni, coordinates za eneo na taarifa za kihistoria zilizopo kabla ya kupendekeza aina ya utafiti unaofaa, huku matokeo yakimsaidia mteja kufanya uamuzi kuhusu hatua inayofuata.
Amesema endapo data za utafiti hazioneshi uwezekano wa kuwepo kwa madini yanayolengwa, kampuni inaweza kumshauri mteja kutotumia fedha zaidi katika eneo hilo, hatua inayoweza kusaidia kupunguza gharama na hasara zinazotokana na uchimbaji usio na taarifa za kutosha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Machimbo Explorer, Omega Nziku, amesema teknolojia inatumika katika hatua mbalimbali za awali kupitia vipimo na baada ya kupata taarifa kutoka kwenye vipimo hivyo, kampuni inaweza kutumia mashine za Diamond Drill na RC katika hatua za uchunguzi wa kina ambao unalenga kusaidia mwekezaji kufanya maamuzi akiwa na taarifa zaidi na kudhibiti gharama, badala ya kuanza kuchimba bila kujua eneo linalofaa.
