Koroo 1 1

Sekta Ya Korosho Yaendelea Kuinua Kipato Cha Wakulima Na Uchumi Wa Tanzania

MUHTASARI


Wabanguaji wadogo katika msimu wa mwaka 2025 walibangua na kuuza korosho zilizofikia thamani ya Sh milioni 34.4.


Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) imeendelea kusimamia mauzo ya korosho ghafi kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.2 (Sh1,202,666,444,600) katika msimu wa mwaka 2025/2026.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile ndc, wakati akitoa hotuba katika Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho uliofanyika mkoani Morogoro.

Brigedia Jenerali Mstaafu Mwanjile alisema katika kipindi hiki cha awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa korosho pamoja na maendeleo katika eneo la ubanguaji na uongezaji thamani wa zao hilo.

Alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano na uwezeshaji unaotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, hususan uamuzi wa kutoa pembejeo za kilimo kwa wakulima bila malipo, hatua ambayo imeongeza tija na kuchochea uzalishaji wa korosho nchini.

Aidha, alisema Bodi imewaajiri vijana 512 kupitia mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora BBT, ambao wamepelekwa katika mikoa inayolima korosho na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuongeza uzalishaji na tija ya zao hilo.

Francis 780x470 1
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Bwn Francis Alfred

Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mstaafu Mwanjile alisema Bodi imesimamia mauzo katika soko la awali kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho nchini, ambapo wabanguaji waliweza kununua korosho ghafi zenye thamani ya takribani Sh. bilioni 29.8.

Alisema Bodi pia imenunua mashine 100 za umeme kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo wanaojihusisha na ubanguaji wa korosho pamoja na vikundi vilivyoanzishwa katika maeneo yao. Mashine hizo zitatolewa bure kwa walengwa kama sehemu ya mpango endelevu wa kuongeza thamani ya zao la korosho.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, wabanguaji wadogo katika msimu wa mwaka 2025 walibangua na kuuza korosho zilizofikia thamani ya Sh milioni 34.4.

“Hili ni eneo muhimu katika uchumi wa nchi. Hivyo, nitoe rai kwa wakulima kuanza kuona ubanguaji kama fursa ya kuongeza thamani ya mazao wanayozalisha badala ya kuuza korosho ghafi,” alisema Brigedia Jenerali Mstaafu Mwanjile.

Alitoa wito kwa wakulima kuongeza juhudi katika ubanguaji wa korosho ili kufikia mwaka 2030, korosho zote zibanguliwe ndani ya nchi. Hatua hiyo, alisema, itaongeza thamani ya zao, kuchochea uwekezaji na kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa CBT Francis Alfred alisema kuwa CBT imeendelea kusambaza miche kwa wakulima bure, ambapo msimu uliopita miche iliyosambazwa ilikuwa milioni 3.2 na msimu mwa mwaka huu wa 2026/2027 inatarajiwa kusambazwa miche milioni 15 huku mpango wa kitaifa ukiwa unalenga uzalishaji wa tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2030.

Nao wakulima wa zao hilo akiwemo Mwanahamis Amiri kutoka wilaya ya Newala, mkoa wa Mtwara alisema uamuzi wa serikali kuwapatia pembejeo za rukuzu kumewapunguzia mzigo na hivyo kuongeza ari ya uzalishaji wa korosho na kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Aliiomba iendelee kuwasaidia wakulima wadogo ambao anachangia kiasi kukubwa cha ukuaji uchumi kwa kuwa ruzuku ya pembejeo na upatikaji wa masoko ya uhakika kumewaondolea kipindi kigumu walichokuwa wakipitia hapo awali.

Kury4703 Previous post Mavunde Azindua Helikopta Ya Kisasa Ya Kampuni Ya Barrick Kwa Ajili Ya Kusaidia Utafiti Wa Kijiolojia
Img 20260904 Wa0004 Next post Kamati Ya Kudumu Ya Bunge Ya Nishati Na Madini Yapatiwa Mafunzo Kuhusu Mikataba Ya Msaada Wa Kiufundi Katika Sekta Ya Madini