MUHTASARI
Helikopta Hiyo Itatumika Pia Kusaidia Tafiti Katika Maeneo Ya Wachimbaji Wadogo Nyamongo, Tarime
Na Damas Makangale/ Nyamongo , Tarime Vijijini
Waziri wa Madini , Anthony Mavunde amezindua helikopta ya kisasa ya kampuni ya Barrick itakayotumika kufanya utafiti wa kijiolojia wa anga kwenye eneo la kilomita za mraba 6,000 pamoja na maeneo ya wachimbaji wadogo katika juhudi za serikali za kuwainua wachimbaji hao na kupunguza athari za mazingira na kuboresha shughuli za utafuta wa madini nchini.
Akizungumza kwenye ghafla ya uzinduzi wa Helikopta hiyo na Programu ya kesho iliyo bora zaidi kwa sekta ya madini (Mining for Brighter Tomorrow ) kwa ajili ya wachimbaji wadogo , Waziri Anthony Mavunde amesema kwamba mahusiano kati ya Mgodi wa Barrick North Mara na wachiimbaji wadogo na wananchi wa mji wa Nyamongo , Wilaya ya Tarime vijjijini unazidi kuimarika kwa pande zote kuanza kufanya kazi kwa pamoja.

Aliongeza kwamba mpango wa kampuni ya Barrick kuongeza nyenzo za kufanya utafiti kwenye eneo lao la kilomita za mraba 6,000 na kwa mita 30 kutoka ardhini ambayo kwa kitaaluma wanaita (High Resolution) itasaidia kujua viashiria vya madini na miamba yenye mipasuko.
“Baada ya mashauriano na uongozi wa Barrick kuhusu namna ya kufanya kazi na wananchi wa maeneo Barrick walikubali kurudisha leseni ya baadhi ya maeneo ambayo walifanya tafiti na kuwapa vijana wa nyamongo kwa ajili ya uchimbaji,”
“Lakini leo hii tunaanza safari ya mafanikio makubwa na vijana wa nyamongo wanaanza uchimbaji wa madini kwa uhakika zaidi baada ya kampuni ya Barrick kukubali kuwapa helikopta yao kwa ajili ya utafiti wa kitalaamu kwenye maeneo yao haya ni mafanikio makubwa kwa vijana , wakinamama na watu wenye ulemavu ,” alisisitiza Waziri Mavunde.
Aliongeza kwamba serikali kupitia Taasisi za Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambayo ilianzishwa tangu 1925 imefanya kazi ya kupima ramani ya madini kwa 97% na utafiti wa kina na mipasuko wa miamba kwa asilimia 16% tu.
“Kutokana na taarifa hizi serikali ya awamu ya sita kupitia Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye alitoa maelekezo ya kutenga asilimia 10% ya mapato yanayotoka kwenye sekta ya madini ili kufanya utafiti wa kina nchini nzima,” Aliongeza Mavunde.

Alisisitiza kwamba sekta ya madini inahitaji uwekezaji kwenye teknolojia na sayansi ili kuweza kufanya utafiti kisasa zaidi kwa kutumia helikopta ili kuleta kasi ya matokeo Chanya pamoja na kuendelea kulinda mazingira.
Pamoja na mambo mengine , Waziri Mavunde akizungumza kuhusu programu ya kesho iliyopo bora kwa sekta ya madini (Mining for Brighter Tomorrow) alisisitiza kwamba ni shauku ya serikali kupitia wizara ya madini kuona kwamba wanawake , vijana na watu wenye ulemavu kuingia na kushiriki zaidi kwenye sekta ya madini nchini.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Barrick nchini , Dkt Melkiory Ngido amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini na kufungua milango ya tafiti kwa kutumia nyenzo za kisasa na kuwashirikisha wachimbaji wadogo ili kupanua mnyororo wa thamani.
Dkt Ngido aliongeza kuwa uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni muhimu katika utekelezaji wa sera ya madini ya Taifa, inayolenga kuimarisha utafiti wa rasilimali madini, kuongeza thamani ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi zaidi huku uchangiaji kwenye maendeleo ya nchini ukiendelea kukua kwa kasi.

“Napenda kuchukua fursa kukushuru Waziri wa madini , Bw Mavunde kwa kila jambo ambalo umekuwa ukiahidi unalitekeleza kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye mapato, ajira na ukuzaji wa mnyororo wa thamani,” alisisitiza Dkt Ngido
Dkt. Melkiory Ngido Aliongeza kwamba kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika shughuli za utafiti wa kisasa wa kijiolojia na maeneo ambayo yatakuwa hayana vigezo kwa uwekezaji mkubwa watarudisha leseni kwa serikali kwa ajili ya kupewa wachimbaji wadogo.
Dkt Ngido pamoja na mambo mengine alichukua nafasi kuishukuru serikali ya mkoa , wilaya na viongozi wa wengine kwa kuboresha mahusiano kati ya mgodi wa Barrick North Mara na vijiji vinavyozunguka mgodi huo kwani mahusiano yameleta tija kwenye ajira , mapato ya halmashauri na maelewano kwenye jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini , Subira Mgalu amesema kwamba programu ya kesho iliyo bora kwa sekta ya madini ni muhimu kwa kupanua wigo wa wanufaika kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Aliogeza kwamba uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya utafiti wa kisayansi wa kijiolojia utaongeza ufanisi kwenye sekta ya madini na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo pamoja na mnyororo wa thamani.
“Nachukua fursa hii kuwashukuru sana kampuni ya Barrick hasa kupitia Mgodi wake wa North Mara kwa kutoa nafasi kwa maeneo ya wachimbaji wadogo kutumia helikopta hiyo ya kisasa kwa ajili ya utafiti wa kisayansi ya jiolojia ya anga (High Resolution airborne geological survey) ambayo kwa hakika utakuwa na tija na matokeo Chanya kwa watanzania,” aliongeza Mgalu.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, alishukuru Wizara ya Madini kwa namna ambavyo imeendendelea kulipa msukumo suala la kuwezesha vijana kushiriki kikamilifu kwenye shughulo za sekta hiyo.
