MUHTASARI
Waziri Kijaji amewaonya askari na maafisa wa uhifadhi kujiepusha na rushwa, ujangili, uvunaji haramu wa misitu na vitendo vingine vinavyohatarisha rasilimali za Taifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka askari na maafisa wa uhifadhi kujenga taswira njema ya Jeshi la Uhifadhi kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu, nidhamu na maadili ya kazi, huku wakiepuka matumizi ya nguvu kupita kiwango kinachohitajika.
Waziri Kijaji ametoa kauli hiyo wakati akifunga rasmi mafunzo ya awali ya kijeshi kwa askari wapya 328 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele, Katavi.

Amesema mafunzo hayo hayakulenga kuwajengea uwezo wa kuvaa sare na kufanya gwaride pekee, bali kuwafanya kuwa watumishi wenye nidhamu, utii, ujasiri, uzalendo na uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja.
Dkt. Kijaji pia amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka na kufuata mnyororo wa utoaji amri (chain of command), akiwataka askari kuwasilisha taarifa za kiutendaji kupitia mamlaka husika na kuepuka kusambaza taarifa nyeti kwenye mitandao ya kijamii.
Aidha, amewaonya askari na maafisa wa uhifadhi kujiepusha na rushwa, ujangili, uvunaji haramu wa misitu na vitendo vingine vinavyohatarisha rasilimali za Taifa, akisisitiza kuwa mtumishi anayehusika na vitendo hivyo anasaliti dhamana na kiapo alichokabidhiwa na Taifa.
Kuhusu matumizi ya nguvu, Waziri amewataka wahifadhi kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo ya ukamataji salama, udhibiti wa hali na matumizi ya nguvu kwa kiwango kinachostahili. Amesema nguvu inapaswa kutumika kwa kuzingatia sheria, taratibu, mazingira ya tukio na kiwango kinachohitajika kutimiza lengo halali la kiutendaji, huku utu wa wananchi ukilindwa.

Waziri Kijaji amesisitiza pia umuhimu wa kujenga urafiki kati ya Jeshi la Uhifadhi na wananchi, akisema jamii ni mdau muhimu katika uhifadhi. Ameelekeza elimu ya uhifadhi kuimarishwa katika jamii, ikiwemo kufundishwa kwa wimbo wa Jeshi la Uhifadhi katika shule za msingi zinazozunguka maeneo ya hifadhi ili kujenga uelewa wa umuhimu wa misitu na rasilimali za asili kwa kizazi kijacho.
“Nendeni mkaitumikie Tanzania kwa moyo mmoja, nendeni mkalinde rasilimali za Taifa letu kwa uaminifu, nendeni mkawa mfano wa nidhamu, uadilifu na uzalendo,” alisema.
