Img 20261002 Wa0082

TARI Na ICIPE Zaongeza  Nguvu Kudhibiti  Wadudu  Waharibifu Wa Matunda

MUHTASARI


Kupitia mradi wa Fruit Tree Agroecological-based IPM katika wilaya za Siha, Hai, na Muheza, wakulima wanafundishwa mbinu mbadala zinazolenga kukata mzunguko wa uzazi wa wadudu na kupunguza matumizi ya viuatilifu vya kemikali.


Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (icipe) cha nchini Kenya, zimeongeza kasi ya kusambaza teknolojia salama za Udhibiti Husishi wa Wadudu (IPM).

Hatua hii inalenga kuokoa mazao ya parachichi, embe, na machungwa mkoani Kilimanjaro na Tanga, maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na uharibifu mkubwa wa nzi na nondo wa matunda.

Tafiti zinaonesha kuwa nzi wa matunda husababisha hadi asilimia 25 ya upotevu wa parachichi katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania, wakati nondo wa matunda akisababisha hasara ya karibu asilimia 40 kwenye machungwa.

Img 20261002 Wa0084
 Wakulima wa parachichi Kata ya Ivaeny Wilayani Siha wakipatiwa mitego ya kunasa wadudu waharibifu wa matunda mara baada ya kupewa mafunzo na watafiti. 

 Kwa muda mrefu, maeneo mengi yamekuwa yakitegemea matumizi makubwa ya kemikali; njia ambayo si salama kwa mazingira, afya ya walaji, na soko la matunda kama hazitatumika kwa usahihi.

Kupitia mradi wa Fruit Tree Agroecological-based IPM katika wilaya za Siha, Hai, na Muheza, wakulima wanafundishwa mbinu mbadala zinazolenga kukata mzunguko wa uzazi wa wadudu hawa na kupunguza matumizi ya viuatilifu vya kemikali.

 Mbinu hizo ni pamoja na; Ukaguzi wa mara kwa mara wa mashamba, Matumizi ya mitego maalum ya kunasa wadudu, Matumizi ya vimeleatilifu hai (biopesticides), Matumizi ya mtego wa chambo cha protini (protein bait) ambao hutumiwa zaidi kudhibiti nzi wa kike wanaohitaji protini kwa ajili ya makuzi ya mayai yao.

Njia nyingine ni usafi wa mashamba kupitia matumizi ya mahema maalum ya kuhifadhi matunda yaliyooza (augmentaria) ili kuzuia wadudu kuzaliana, na pia matumizi ya wadudu jamii ya nyigu aina ya Diachasmimorpha longicaudata (DL) na Fopius arisanus chini ya uratibu wa mamlaka husika. 

Mbinu hii ya kibaolojia inatumika kudhibiti nzi wa matunda (fruit flies) ambao wanaharibu maembe, machungwa, na parachichi, pamoja na baadhi ya mboga-matunda.

Ili kuhakikisha uendelevu wa mradi huu unaofadhiliwa na shirika la GIZ kupitia ICIPE, mnamo Septemba 27 na 28, 2026, jumla ya wakulima 259 wa Wilaya za Siha na Hai walipata mafunzo ya vitendo na kugawiwa mitego ya kunasa nzi wa matunda. 

Mafunzo hayo yalihusisha pia maafisa ugani na  kampuni ya Elephant Vert ya mkoani Arusha, ambayo inazalisha na kusambaza mitego na vimelea tilifu. 

Lengo la kuwakutanisha wakulima na wasambazaji wa pembejeo ni kurahisisha upatikanaji wa vifaa na teknolojia hizo salama. Wakulima waliohudhuria wamepongeza juhudi hizo na kuomba watafiti kusogeza elimu hiyo kwenye kata ambazo bado hazijafikiwa.

Akitolea ufafanuzi hatua zinazofuata, Mtafiti Kiongozi wa mradi huo kutoka TARI, Dkt. Abdullah Mkiga amesema teknolojia hizi kila mkulima akizitumia ni rahisi kudhibiti changamoto ya wadudu waharibifu kwa upana zaidi (Areawide control). 

Img 20261002 Wa0083
 Watafiti wakionesha kwa vitendo namna ya kuhifadhi matunda yaliyooza kwa kutumia hema maalum.

“Tunapanga kupanua wigo wa mradi huu ili tuwafikie wakulima wengi zaidi. Katika maeneo ambayo tayari tumeshafundisha, tumeona wakulima wameelewa na tumewaunganisha na wasambazaji wa pembejeo.” Amesema.

Watafiti wakionesha kwa vitendo namna ya kuhifadhi matunda yaliyooza kwa kutumia hema maalum

Img 20261002 Wa0025 Previous post Deni La Taifa Ni Himilivu – Benki Ya Dunia 
Img 20261003 Wa0006 Next post TFS Yashiriki Usafi, Upandaji Miti World Cleanup Day Wilaya Ya Kondoa, Dodoma