O0a06411

Mhandisi Innocent Masaka: Mtaalamu Kijana Wa Kilimo Aliyebeba Maono Ya Kuipa ASA Muelekeo Mpya

“Mwenye Maono Huona Mbali, Mwenye Hekima Hujua Njia, Na Mwenye Uthubutu Huanza Safari.


WAKALA wa Mbegu za Kilimo Tanzania (ASA), ni miongoni mwa taasi muhimu sana katika kuliwezesha Taifa la Tanzania kuyafikia maono chanya ya kuwa na utoshelevu wa chakula nchini kwa kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara yanayostawi katika mikoa mbalimbali.

Aidha, ni dhahiri kuwa, maono ya Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2050 hayawezi kufikiwa kama wakulima nchini hawatapata mbegu bora za kutosha kwa wakati.

Adhali za mabadilko ya Tabia Nchi ni changamoto nyingine inayoonekana kufifisha maono haya mazuri kama serikali haitajikita katika kuweka miundombinu mizuri ya umwagiliaji ili kuwawezesha wazalishaji wa mbegu kuzalisha mbegu bora mwaka mzima bila kutegemea maji ya mvua.

Takwimu za sekta ya mbegu nchini Tanzania zinathibitisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa upatikanaji wa mbegu bora, ikiwa ni dhidi ya ongezeko kubwa la uhitaji wa mbegu hizo nchini.

Kwa sasa, nchi inahitaji angalau tani 127,000 za mbegu kwa mwaka ili kukidhi uhitaji, lakini kiasi kinachozalishwa hadi sasa kipo chini ya asilimia 50 ya uhitaji huo.

Kwa kuwa kilimo ni sekta mama kwa uchumi wa Tanzania, imeaajiri zaidi ya asilimia 65 ya nguvukazi ya Watanzania, na inachangia takriban asilimia 26 hadi 28 kwenye Pato la Taifa (GDP), ni ukweli usiopingika kuwa hata maono ya Dira ya Maendeleo 2050 hayatawezekanika pasipo matokeo chanya kwenye sekta ya kilimo.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Chapisho hili, Bwn Valentine Oforo, amepata fursa ya kufanya mahojiano ya kina na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa ASA, Mhandishi Innocent Masaka, kwa lengo la kujua ana maono gani ya kuipa Taasisi hiyo ya Serikali meno mapya ya kuhakikisha uzalishaji wa mbegu bora unaongezeka, na wakulima nchini wanapata mbegu hizo kwa wakati sahihi.

4 Asa 061426
Mhandisi Innocent Masaka

SWALI: Ulijisikiaje ulipopokea taarifa za uteuzi wako?

JIBU: Nilishangaa, lakini pia nilifurahi sana. Kuongoza taasisi muhimu kama hii, ambayo ina nafasi kubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini Tanzania, na inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa, si jukumu rahisi. Lakini namshukuru Mungu, kwa sababu naamini ndiye aliyekuwa nyuma ya uteuzi wangu.

Pia, ninamshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, kwa kuniamini kuwa mtu sahihi wa kuvaa viatu hivi.

SWALI: Uliikuta ASA katika hali gani ulipoanza kazi? Je, ulikuta Wakala ukiwa katika hali nzuri au ulikumbana moja kwa moja na changamoto kadhaa?

JIBU: Hapana, niliikuta Wakala ikiwa katika hali nzuri. Watangulizi wangu, Dkt Sophia Kashenge, na Dkt Leo Mavika walifanya kazi kubwa kuhakikisha ASA inatoa huduma zake kwa ufanisi na inaendesha shughuli zake kwa mpangilio mzuri. Wakulima walikuwa wakipata mbegu bora kwa kiwango cha kutosha na, jambo muhimu zaidi, kwa wakati unaofaa.

Kwa hiyo, jukumu langu sasa ni kuendeleza, na kuyajenga maono yangu juu ya msingi huo imara niliyoukuta tayari umewekwa.

Kimsingi, maono yangu yanajikita katika kuibadilisha ASA kuwa wakala unaozingatia zaidi biashara na unaoweza kujiendesha kibiashara kwa uendelevu. 

Lengo letu ni kuongeza zaidi uzalishaji wa mbegu, kuboresha ufanisi na kuhakikisha wakulima katika maeneo yote ya kilimo nchini Tanzania wanapata mbegu bora na zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.

SWALI: Umejiwekea mkakati gani kufikia malengo hayo?

JIBU: Kimsingi, ASA imepewa jukumu la kuzalisha mbegu bora na kuzisambaza kwa wakulima kwa bei elekezi iliyowekwa na Serikali. Jukumu jingine muhimu ni kutoa elimu na kuhamasisha wakulima kuhusu faida za kutumia mbegu bora ambazo zimeidhinishwa na Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI). Pia tumepewa jukumu la kufanya tafiti za kina kuhusu mahitaji ya mbegu bora nchini.

Jukumu letu jingine ni kuwahamasisha wadau wa sekta binafsi kushiriki katika uzalishaji mbegu bora ili kuweza kukidhi uhitaji.

Watangulizi wangu wamekuwa wakitekeleza majukumu haya kwa bidii ili kuhakikisha malengo hayo muhimu yanafikiwa. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya mambo ambayo hayajakamilika, hivyo ni jukumu langu kuyashughulikia.

Kwa hiyo, kutokana na swali lako, maono yangu yanajikita katika maeneo yafuatayo ili kuhakikisha Wakala unatoa huduma kwa kuendana na matarajio ya Serikali.

Kwanza, nitafanya kazi ya kuendelea kuboresha uwekaji wa mifumo ya kisasa ya umwagiliaji katika mashamba yote ya mbegu na kuhakikisha mifumo hiyo inafanya kazi kwa ufanisi na kwa uendelevu. 

Hii itaiwezesha ASA kutumia kikamilifu mashamba yake yote yanayozalisha mbegu, kwa kulenga kufikia matumizi ya asilimia 100 ya mashamba hayo. Pia, lengo ni kuhakikisha mashamba yote yanaweza kufikika na kuzalisha mbegu mwaka mzima (kipindi cha mvua, na kiangazi).

Pia, nitajitahidi kuongeza wigo wa ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu. Tunakusudia kuingia mikataba na kampuni nyingi zaidi za mbegu pamoja na wakulima wa mkataba ili kuongeza kasi na kiwango cha uzalishaji wa mbegu.

Serikali inafanya kazi kuhakikisha sekta ya kilimo nchini Tanzania haizalishi kwa ajili ya mahitaji ya ndani pekee, bali pia inazalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya kulisha nchi nyingine. Ili kutimiza azma hii ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, wakulima wetu lazima wajikite kwa dhati katika kilimo biashara, na hilo linahitaji upatikanaji wa mbegu bora za kutosha.

SWALI: Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa mbegu bora, huku mahitaji yakiwa makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji. Utafanya nini kuiweka ASA katika nafasi nzuri zaidi ya kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuziba pengo hili?

JIBU: Ni kweli. Mahitaji ya mbegu bora nchini Tanzania yanakadiriwa kufikia takribani tani 127,000 kwa mwaka, lakini uzalishaji wa sasa ni chini ya asilimia 50 ya mahitaji halisi.

Kitu ninachotaka kukiona kwa dhati ni ASA kuweza kuuza kwa wakulima nchini kote kiasi chote cha mbegu inachozalisha. Kwa sasa, mbegu zinazozalishwa na kampuni binafsi, ASA na wakulima wa mkataba, bado hazitoshelezi mahitaji ya nchi.

Lakini, wakulima wengi pia wamekuwa wakielezea juu ya upatikanaji na usambazaji hafifu wa mbegu bora katika maeneo mbalimbali nchini. 

Ili kukabiliana na changamoto hii, kama nilivyosema awali, tutaongeza uzalishaji na kuhakikisha ASA inatambulika na watumiaji wote kama chanzo cha kuaminika cha mbegu bora nchini.

SWALI: Una mipango gani mingine ya kubadilisha uendeshaji wa ASA?

JIBU: Sawa, asante kwa swali zuri. ASA ni taasisi inayomilikiwa na Serikali ambayo kimsingi hutoa huduma, lakini kwa uhalisia pia tunajihusisha na biashara, huku Serikali ikitupatia ruzuku.

Lengo langu ni kuibadilisha ASA kuwa taasisi inayolenga kikamilifu biashara, kiasi kwamba iweze kujiendesha kwa kutumia rasilimali zake za kifedha na kuanza kuirudishia Serikali sehemu ya mapato yake kupitia malipo ya gawio.

Najua hii ni safari ndefu na ngumu, lakini inawezekana. Nina watumishi wenye uwezo na walio tayari kufanya kazi. Kinachohitajika ni kubadili mtazamo wetu na kuwa na dhamira kubwa ya kufikia lengo hili.

SWALI: Tanzania inakabiliwa na upungufu wa takribani tani 350,000 za mafuta ya kula kwa mwaka, changamoto ambayo inailazimimu nchi kutumia wastani wa Dola za Marekani milioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka. Una mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya mafuta ya kula kama alizeti, mawese, karanga na ufuta?

JIBU: Ni kweli kabisa kwamba Tanzania ina upungufu mkubwa wa mafuta ya kula, na ASA ni miongoni mwa taasisi muhimu zinazoweza kusaidia nchi kukabiliana na changamoto hii, hasa kupitia uzalishaji wa mbegu bora za mazao yanayozalisha mafuta ya kula, jambo litakalowawezesha wakulima na wachakataji kuongeza uzalishaji.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba kwa sasa ASA inajikita katika kuzalisha aina za mbegu za mazao ambayo Serikali imeyapa kipaumbele kama mazao ya kimkakati.

Kuhusu swala la uhaba wa mafuta ya kula, hadi sasa tumeshatengeneza mfumo unaotekelezeka wa kuongeza uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za alizeti. Kwa mfano, katika msimu huu, Wakala unatarajia kuzalisha kati ya tani 1,200 na 1,300 za mbegu za mazao yanayozalisha mafuta ya kula, wakati msimu ujao uzalishaji unatarajiwa kufikia hadi tani 1,900.

Kimsingi, tunatakiwa kuongeza uzalishaji hadi angalau tani 2,500 ili kuiweka nchi katika nafasi nzuri zaidi ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya mafuta ya kula.

 

F488c Mahindi2b2
 

Aidha, kwa mujibu wa malengo ya Serikali, Wakala unatakiwa kuongeza uzalishaji wa mbegu kwa ujumla hadi kufikia tani 28,500 ifikapo mwaka 2030.

Na ili kuhakikisha mbegu hizo za mazao ya uzalishaji wa mafuta zinawafikia wakulima wote kwa wakati, tunafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mengine (COPRA), pamoja na wadau wengine muhimi.

SWALI: Dunia kwa sasa inashuhudia mapinduzi na matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa katika sekta ya kilimo. Una mikakati gani wa kuhakikisha ASA inaendana na kutumia kikamilifu teknolojia hizo, ikiwemo Akili Unde (AI), ili kuboresha utoaji wa huduma?

JIBU: ASA tayari imeanza kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia duniani. Kwa mfano, tayari tumeweka, na tutaendelea kuweka, miundombinu ya teknolojia za hali ya juu katika mashamba yetu ya mbegu, yakiwemo yale yaliyo chini ya mifumo ya umwagiliaji.

Kwa sasa tunafanya kazi kuelekea kuweka shughuli zetu zote katika mfumo wa kidijitali, kuanzia ofisini hadi mashambani. Maono yetu ni kuharakisha na kuweka viwango bora katika utoaji wa huduma zetu, lengo ni kuhakikisha taratibu zote zinazohusisha wakulima wa mkataba, ushirikiano na kampuni binafsi za mbegu, pamoja na ufuatiliaji wa mnyororo mzima wa mbegu wa ASA zinafanyika kidijitali.

SWALI: Sekta ya kilimo Tanzania inakabiliwa na changamoto ya mbegu feki zinazouzwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu. Mkakati wako utakuwa upi kuhakikisha ASA inafanya kazi kwa karibu na TOSCI kuziba mianya inayoruhusu uuzaji wa mbegu zisizo na viwango kwa wakulima nchini?

JIBU: Udanganyifu ni suala ambalo limeonekana kuwepo katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, katika sekta ya mbegu, wale wanaohusika na vitendo hivyo vya ukiukwaji wanabainishwa na kuchukuliwa hatua.

Moja ya mambo muhimu nitakayofanya ni kuimarisha zaidi uhusiano wetu wa kikazi na TOSCI katika eneo hili. Kwa kufanya hivyo, wakulima wengi zaidi watapatiwa elimu kuhusu namna ya kutambua mbegu zisizo na ubora. TOSCI tayari imeanzisha mifumo ya kidijitali inayowawezesha wakulima kuhakiki uhalali wa mbegu kwa kutumia simu janja na simu za kawaida. Kinachohitajika sasa ni mpango madhubuti wa kuwaelimisha wakulima na wafanyabiashara wa mbegu namna ya kutumia mifumo hiyo.

Hatua nyingine muhimu ya kumaliza tatizo hili ni kuhakikisha kuwa mbegu bora za kutosha zinazalishwa na kusambazwa kwa ufanisi hadi kuwafikia wakulima. Nina matumaini makubwa kwamba tutashinda changamoto hii, kwa sababu mipango ipo ya kuifanya ASA iingie mikataba na mawakala wakubwa na wenye utaalamu wa usambazaji wa mbegu katika maeneo yote nchini. Wasambazaji hao watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata, kijiji, mtaa hadi kaya.

Kama sehemu ya juhudi hizi, pia tutafanya kazi kwa karibu na Wakala wa Huduma za Ugani wa Kilimo Tanzania (NAESA). Hii ni taasisi mpya iliyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kupanua utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima katika ngazi zote nchini. 

Lengo letu ni kutumia maafisa ugani wa NAESA, ambao wamesambaa katika maeneo mbalimbali nchini, kama mabalozi wazuri wa kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora na zilizoidhinishwa.

Mpango mwingine wa kukabiliana na changamoto ya mbegu bandia ni kufanya kazi na Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC). TFC inasimamia vyama vya wakulima vikubwa na vidogo vyote, kote nchini.

Kwa kuwa vyama hivi vina maduka yao ya pembejeo za kilimo, hivyo kufanya kazi kwa karibu na TFC kutatoa njia nyingine ya kuaminika ya kuhakikisha wakulima wanapata na kutumia mbegu zilizoidhinishwa.

SWALI: ASA ina nafasi gani katika kuchangia juhudi za Tanzania kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050?

JIBU: Kwa hakika, ASA ina nafasi muhimu sana, tukizingatia umuhimu wa mbegu bora katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inafanya kazi kufikia lengo la kuhakikisha sekta ya kilimo inafikia ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2050.

Malengo yote haya yanahitaji uzalishaji na usambazaji wa aina bora za mbegu kwa mazao yote ya kimkakati nchini Tanzania.

Maono yangu makubwa ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2050, ASA inakuwa taasisi kubwa ya kibiashara yenye uwezo wa kuzalisha mbegu kulingana na mahitaji yanayoongezeka nchini, huku ikiweza kujiendesha kwa kutumia rasilimali zake za ndani za kifedha na kuchangia katika uchumi wa taifa.

E181cab1 3bdb 4743 Aa88 436ad0ab50af 780x470 1 Previous post UZINDUZI WA JNHPP: Tanzania Kuandika Historia Mpya Kwenye Uzalishaji Umeme
Img 20260824 Wa0015 Next post Msaada Wa TFS Wa Madawati Yenye Thamani Ya Sh Milioni 7 Waweka Tabasamu Kwa Wanafunzi Ifakara