Img F8b631c5 2120 4794 8012 85b575263e22

Wakulima 8,000 Kunufaika Na Awamu Ya Pili Ya Utekelezaji Wa Mradi Wa Kilimo Thabiti 

MUHTASARI


Matumizi ya mifumo ya kidijitali katika mradi wa Kilimo Thabiti  yamekuwa na msaada mkubwa kwa wakulima wanufaika


Na Valentine Oforo

Awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo Thabiti imezinduliwa Mkoani Mara, ukitarajia kuwanufaisha takribani wakulima wapatao 8,000 katika halmashauri za Wilaya za Musoma Vijijini, Bunda, Butiama, na Serengeti.

Mradi wa Kilimo Thabiti unalenga kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa kidijitali na ushauri wa kilimo kwa wakulima wadogo kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kulingana na maeneo walipo, pamoja na kushauri mbinu bora za kilimo kwa eneo husika ili hatimaye kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Sehemu ya Utawala na Utumishi Mkoa wa Mara, Ndg. Dominicus Lusasi, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kama Mgeni Rasmi, amesema kuendelea kwa mradi huo ni ishara ya kuongezeka kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto za kilimo.

Img 20260924 Wa0063
Mkurugenzi mtendaji wa TYEGD Ndg. Benjamin Kadikilo  akitoa taarifa ya mafanikio yaliyofikiwa  katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo Thabiti kabla ya ufunguzi wa awamu ya pili ya mradi huo.

Amesisitiza kuwa serikali ya mkoa itasimamia na kutoa ushirikiano wa kutosha katika awamu hii ya pili. Pia, Ndg. Lusasi ametoa wito kwa washiriki wote wa mradi kuhakikisha uendelevu wake hata baada ya ufadhili kukoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Deusdedith Mbanzibwa, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika mradi huu yamekuwa na msaada mkubwa kwa wakulima, hatua ambayo imeleta chachu kwa taasisi hiyo kuongeza nguvu katika matumizi ya TEHAMA wakati wa utekelezaji wa miradi mingine.

Baadhi ya wanufaika wa awamu ya kwanza ya mradi wamepongeza wadau wote walioshiriki kuasisi mradi huo ambao umewasaidia katika uandaaji wa mashamba, utunzaji wa mazao yakiwa shambani, uvunaji, na pia usimamizi wa mazao baada ya mavuno.

“Binafsi nimepata faida kubwa kwenye mradi wa Kilimo Thabiti. Nilikuwa nikipata ujumbe mfupi kuhusu kuandaa mashamba kwa wakati kutokana na hali ya hewa iliyotabiriwa, hatua iliyosaidia pia wakulima wengine ambao nilikuwa nikiwapa taarifa hizo za utabiri wa hali ya hewa,” amesema Ndg. Breck Amos, mkulima kutoka kijiji cha Nyangere, kata ya Nyamang’uta Wilayani Bunda.

Naye Bi. Frolentina Manyama, mkulima kutoka kijiji cha Nyakiswa Wilayani Bunda, ametoa ombi la kuongezwa kwa idadi ya wanufaika ili wakulima wengi zaidi waweze kupata taarifa za hali ya hewa na ushauri wa kilimo kwa wakati.

Img 20260924 Wa0061
 Baadhi ya wadau wakitoa maoni yao kuhusu vipaumbele katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo Thabiti.

Awamu ya pili ya utekelezaji wa Mradi wa Kilimo Thabiti imekuja wakati ambao Tanzania imeanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayoweka msisitizo katika kuongeza tija, matumizi ya teknolojia, ubunifu, uongezaji thamani wa mazao, na kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ili hatimaye kukuza sekta ya kilimo yenye tija kwa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mradi wa Kilimo Thabiti unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), shirika la Tanzania Youth Espouse for Gender and Development (TYEGD), Esoko, Weather Impact, na maafisa ugani kutoka mamlaka za serikali za mitaa, chini ya ufadhili wa FID.

Katika awamu hii ya pili itakayodumu kwa miaka mitatu, takribani wakulima 8,000 wanatarajiwa kufikiwa.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi, jumla ya wakulima 2,656 walifikiwa na huduma ya ujumbe mfupi kuhusu hali ya hewa, wakulima 541 walifikiwa na mafunzo ya kanuni bora za kilimo, na pia wakulima 30 walipewa mafunzo na kuwa wakulima wanasayansi ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kukusanya taarifa za hali ya unyevu wa udongo.

Img 20260923 Wa0043 Previous post Kamati Ya Bunge Ya Ustawi Na Maendeleo Ya Jamii Yaipongeza Barrick Bulyanhulu Kuzingatia Kanuni Za Afya Na Usalama Mahali Pa Kazi
Img 20260924 Wa0085 Next post Wakala Wa Misitu Tanzania Yataka Watumishi Kuimarisha Uadilifu, Usimamizi Wa Vihatarishi