MUHTASARI
Vihatarishi vyenye athari kubwa vinapaswa kutambuliwa mapema na kupewa kipaumbele katika mipango na bajeti ya Taasisi.
Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini wametakiwa kuzingatia uadilifu, nidhamu, bidii na kufuata sheria, kanuni na miongozo katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi wa taasisi katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za misitu na nyuki.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Kanda ya Kaskazini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, SACC James Nshare, wakati akifungua kikao cha kupitia Daftari la Viashiria Hatarishi (Risk Register) kinachofanyika wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

SACC Nshare amesema usimamizi wa viashiria hatarishi ni jukumu la kila mtumishi na kuwataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha elimu wanayoipata inawafikia watumishi wengine katika vituo vyao, ili kusaidia kutambua, kupunguza na kuondoa vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya TFS.
Amesema vihatarishi vyenye athari kubwa vinapaswa kutambuliwa mapema na kupewa kipaumbele katika mipango na bajeti ya taasisi, akitoa mfano wa maeneo ya utalii ambapo ni muhimu kutambua wanyama na viumbe hatarishi, pamoja na kuweka maandalizi na vifaa vya kukabiliana na dharura.
“Masuala tunayojifunza ni muhimu sana katika taasisi, hivyo ni vema elimu hii ikawafikia wengi. Lazima pia tuhakikishe maeneo yetu ya utalii yanaainisha viashiria hatarishi na kuweka vifaa vya kudhibiti dharura. Mfano, mtu akiumwa na nyoka, tuwe tumejipanga na dawa za kuondoa sumu,” amesema.
Aidha, SACC Nshare amewataka watumishi kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa, kwa kutathmini vihatarishi vilivyopo katika maeneo yao ya kazi na kuchukua hatua stahiki kulinda maisha ya watumishi, wananchi na mali za taasisi.
Awali, Mratibu wa Masuala ya Viashiria Hatarishi TFS, Mhifadhi Mkuu TFS, PCO Mariam Mrutu, amesema utambuzi na uainishaji wa vihatarishi ni muhimu katika kuhakikisha taasisi inafikia malengo yake, na kuwataka watumishi kuainisha vihatarishi katika maeneo yao ya kazi na kutenga rasilimali kwa ajili ya kudhibiti vile vyenye athari kubwa.

Kikao hicho cha siku tano kinawakutanisha wahifadhi kutoka vituo vya TFS vya Kanda ya Kaskazini, mashamba ya miti, sekta ya nyuki na Kituo cha Mbegu za Miti, na kinatarajiwa kuhitimishwa Septemba 27, 2026.
