Img 20260824 Wa0015

Msaada Wa TFS Wa Madawati Yenye Thamani Ya Sh Milioni 7 Waweka Tabasamu Kwa Wanafunzi Ifakara

 

Na Mwandishi Wetu – Morogoro

KATIKA hatua ya kizalendo ya utekelezaji mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Wakala Wa Misitu Tanzania (TFS), imekabidhi madawati mapya 50 yenye thamani ya Shilingi milioni saba kwa Shule ya Msingi Signal, Ifakara.

Msaada huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi katika shule hiyo iliyopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mkoa wa Morogoro.

Img 20260824 Wa0002

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya madawati hayo, Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kilombero, SCO Zarina Shaweji, amesema TFS inatambua na kuthamini mchango wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya misitu katika kulinda na kuhifadhi rasilimali hizo, hivyo imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa lengo la kurejesha kwa jamii.

Shaweji amesema ushirikiano kati ya wananchi na TFS ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za misitu zinaendelea kulindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. 

Amewataka wakazi wa Kijiji cha Signal, kinachopakana na Msitu wa Hifadhi wa Nyanganje, kuendelea kushirikiana na TFS katika kulinda na kutunza misitu pamoja na rasilimali za nyuki.

Aidha, amewataka wanafunzi, walimu na wazazi kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa ili yadumu na kuendelea kutoa huduma kwa wanafunzi wa sasa na watakaokuja baadaye, akisisitiza kuwa mazingira bora ya kujifunzia ni sehemu muhimu ya kuimarisha elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Signal, Jeremia Lembile Sailutye, ameishukuru TFS kwa msaada huo, akisema umesaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. 

“Tunawashukuru sana TFS kwa ajili ya msaada huu uliyokuja kwa wakati muafaka, kwani awali baadhi ya wanafunzi walikabiliwa na changamoto ya kukaa kwa kubanana, hali iliyokuwa ilikuwa ikiathiri utulivu wao darasani na wakati mwingine kuwapa walimu ugumu wa kufundisha kwa ufanisi,” alieleza.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, Mwajuma Nasoro amesema madawati hayo yatasaidia katika kuboresha ufaulu kwa wanafunzi.

“Tunawashukuru sana TFS kwa kutupatia madawati haya 50, tunaahidi kwamba tutayatunza ili yaendelee kuwa na manufaa kwetu na kwa wanafunzi wengine,” alishukuru.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Bwn Abubakar Asenga, ameishukuru TFS kwa msaada huo, na kusema juhudi za taasisi hiyo kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya misitu ni muhimu katika kujenga uhusiano mzuri kati ya wananchi na taasisi za uhifadhi. 

Img 20260824 Wa0006

Aidha, amesema Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa maeneo yanayofanya vizuri katika uhifadhi wa misitu, huku akiiomba TFS kuendelea kushirikiana na jamii katika kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo elimu.

KUHUSU TFS

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS – Tanzania Forest Services Agency) ni wakala wa serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii unaosimamia rasilimali za misitu na nyuki nchini.

Kazi na Majukumu Makuu ya TFS

Uhifadhi na Usimamizi: Kusimamia hifadhi za misitu ya serikali, misitu ya asili, na mashamba ya miti ya kupanda.

Rasilimali za Nyuki: Kuendeleza na kusimamia rasilimali za ufugaji nyuki na mazao yake nchini.

Kukuza Utalii-Ikolojia: Kuendeleza maeneo ya misitu ili kukuza utalii wa asili na kuvutia wageni (unayotajwa kuwa nguzo kuu au sleeping giant wa utalii).

Biashara ya Kaboni na Mapato: Kuongeza mapato yasiyo ya kodi kupitia uvunaji endelevu wa miti, biashara ya kaboni, na ada za maliasili.

Uhifadhi wa Mazingira: Kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni.

O0a06411 Previous post Mhandisi Innocent Masaka: Mtaalamu Kijana Wa Kilimo Aliyebeba Maono Ya Kuipa ASA Muelekeo Mpya
Img 20260826 Wa0002 Next post Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar Chabuni Teknolojia Za Kuwasaidia Wavuvi na Wachimbaji Madini Tanzania