MUHTASARI
“Ushirikiano wa kweli kati ya wawekezaji, wafanyabiashara na Serikali utajengwa kwenye misingi ya mifumo madhubuti ya kikodi , kisera , kikanuni na sheria nchini ndani na kwenye nchi nyinginezo za Afrika Mashariki,”Bwn Rostam Azizi
Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Taifa Group , Bwn Rostam Azizi amesisitiza kuwa uwepo wa utawala bora, Taasisi madhubuti, sera zinazotekelezeka na uwazi wa mifumo vitafungua fursa za uwekezaji na mitaji ya kimataifa ndani ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.
Akiongea kwenye Jukwaa la Nne la Biashara la Watendaji wakuu 200 (200 CEOs Business Forum) linalowakutanisha pamoja wafanyabiashara na wawekezaji nchini, Bwn Azizi amesema ushirikiano wa kweli kati ya wawekezaji , wafanyabiashara na Serikali utajengwa kwenye misingi ya mifumo madhubuti ya kikodi , kisera , kikanuni na sheria nchini ndani na kwenye nchi nyinginezo za Afrika Mashariki.

Aidha, aliongeza kwamba ni muhimu maamuzi katika mkutano huo yalete majawabu juu ya sehemu, na sekta ipi ambayo mitaji inapaswa kupelekwa.
“Rasilimali nyingi za asili , idadi ya watu na eneo la kijiografia havitoshi kuhakikisha uwekezaji wa muda mrefu kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa kuja kuwekeza bali uhakika, utulivu , ukuaji na kujenga imani kwa wawekezaji,” Alisema.
Alisisitiza kuwa ni muhimu mkutano huo kuwa chumba ambacho maamuzi yake yanaleta matokeo chanya katika nyanja ya utekelezaji wa mitaji, pamoja na kujua sekta zinazokua na jinsi ya kutengeneza ajira mpya ndani ya Afrikaa Mashariki.
