Img 20260922 Wa0044

Tanzania Sasa Mwenyekiti Mwenza Katika Jukwaa la Mawaziri Beijin

MUHTASARI


Tanzania na China zina historia ya muda mrefu ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo reli ya TAZARA na usafiri wa majini kupitia SINOTASHIP, huku nafasi hiyo ya Uwenyekiti Mwenza ikitarajiwa kuongeza fursa za kuimarisha ushirikiano huo.


TANZANIA imepewa nafasi ya Uwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi linalofanyika jijini Beijing, China, ambapo Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameongoza kwa pamoja na Waziri wa Uchukuzi wa China, Liu Wei.

Jukwaa hilo la siku tatu limewakutanisha zaidi ya Mawaziri 20 wa Uchukuzi kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujadili maendeleo ya sekta hiyo, kubadilishana uzoefu na kuimarisha miundombinu pamoja na huduma za usafirishaji.

Img 20260922 Wa0045
 

Akizungumza katika jukwaa hilo, Prof. Mbarawa amesema Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika reli ya kisasa, barabara, bandari na viwanja vya ndege kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo pia unalenga kuunganisha maeneo ya vijijini na mijini, kuchochea biashara na kuongeza fursa za kiuchumi nchini.

Aidha, Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kualika taasisi za serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza nchini, akisema sekta ya uchukuzi ina fursa mbalimbali za uwekezaji.

“Tanzania ina fursa nyingi kupitia Sekta ya Uchukuzi, hivyo ninawaalika taasisi za serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya Uchukuzi Tanzania,” amesema.

Ushiriki wa Tanzania katika jukwa hilo unaipa fursa ya kushirikisha uzoefu wake, kujifunza teknolojia na mbinu kutoka nchi nyingine, pamoja na kutafuta fursa za uwekezaji katika miradi ya uchukuzi.

Img 20260922 Wa0046

Jukwaa hilo pia linahamasisha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa China wa Global Development Initiative (GDI), huku Tanzania ikipata nafasi ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika miundombinu, teknolojia na uwekezaji.

Tanzania na China zina historia ya muda mrefu ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi, ikiwemo reli ya TAZARA na usafiri wa majini kupitia SINOTASHIP, huku nafasi hiyo ya Uwenyekiti Mwenza ikitarajiwa kuongeza fursa za kuimarisha ushirikiano huo.

Img 20260910 Wa0014 Previous post Agro Stakeholders Launch Tanzania Agroforestry Platform to Tackle Climate Change, Boost Productivity
Img 20260923 Wa0043 Next post Kamati Ya Bunge Ya Ustawi Na Maendeleo Ya Jamii Yaipongeza Barrick Bulyanhulu Kuzingatia Kanuni Za Afya Na Usalama Mahali Pa Kazi